Thursday, November 8, 2012

HIT SONG YA BEN POL - NIKIKUPATA


Watawa zaidi wajiteketeza kupinga China

8 Novemba, 2012 - Saa 14:09 GMT

Mtawa aliyejiteketeza kuonyesha kero na China
Wanaharakati nchini China wanasema kuwa vijana watatu watawa wa Tibet pamoja na mama mmoja walijiteketeza mkesha wa kongamano la chama cha tawala cha kikomunisti nchini China.
Shrika la Free Tibet linasema kuwa mmoja wa watawa hao alifariki katika kile inachosema ni idadi kubwa ya watu kujiteketeza kama njia ya kuonyesha kukerwa na utawala wa china.
Matukio ya hivi karibuni ya watu kujiteketeza moto katika maeneo ya china yaliyo na watu wa Tibet yamefikisha idadi ya watu hao wanaojiteketeza kuwa zaidi ya watu sitini tangu mwaka jana.
Wengi wao wamefariki. Na huenda kuna umuhimu katika wakati ambapo visa hivi vimetokea.
Kuimarishwa kwa usalama kote China kwa kongamano la chama tawala cha kikomyunisti nchini, hakujazuia malalamiko ya raia wa Tibet dhidi ya utawala wa China. Badala yake yameongezeka.
Wanaharakati wanasema idadi ya watu kujiteketeza kwa muda wa siku moja, hii leo, haikutarajiwa.
Tangu mwaka jana zaidi ya raia sitini wa Tibet wameamua kutumia njia kubwa kabisa ya kuonyesha kuvunjwa moyo, kwa kile wanachosema ni ukandamizaji wa China kwa tamaduni zao.
Raia wa Tibet wanaopinga China
Maafisa wa serikali wa China wametoa fedha katika maeneo yaliyo na raia wa Tibet na wameendelea kukana tuhuma hizo za ukandamizaji.
Mkurugenzi wa kundi linalotetea kuachiwa huru maeneo ya Tibet, amesema malalamiko ya hivi karibuni yananuiwa kutoa ishara kwa kizazi kipya cha uongozi China, kitakachoidhinishwa katika kongamano linaloendelea Beijing, kuwa raia wa Tibet wataendelea kupigania uhuru wao.
Baadhi ya raia wa Tibet walio uhamishoni, wanatumai kuwa mwanamume anayedokezwa kuwa kiongozi mpya, Xi Jinping, huenda akawapatia nafasi ya kufanyika mabadiliko.

Shughuli za uokoaji zashika kasi Ghana

8 Novemba, 2012 - Saa 15:43 GMT

Shughuli za uokoaji zashika kasi Ghana
Shughuli za uokoaji ili kutafuta manusuru zingali zinaendelea katika jengo lililoporomoka jijini Accra, mji mkuu wa Ghana.
Jengo hilo, lililokuwa na orofa kadhaa, liliporomoka siku ya Jumatano. Jengo hilo lilikuwa limekodishwa na duka la Melcom, na lilifunguliwa mapema mwaka huu.
Mwandishi wa BBC, Sammy Darko, anayeripoti kutoka eneo la tukio, anasema anaona mikono ya watu watatu ikitokezea kutoka maporomokoni, huku waokoaji wakijitahdidi kuwafikia.
Hadi sasa watu watano wamethibitishwa kufariki, huku wengine 65 wakiokolewa wakiwa hai.
Rais John Dramani amesitisha kwa muda kampeni zake za urais, huku akitangaza eneo la tukio kuwa eneo la janga. Pia, aliamuru uchunguzi kuhusu kilichosababisha mkasa huo, ufanywe.
Kikundi cha Waisraeli kinategemewa kuwasili Alhamisi ili kusaidia katika juhudi hizo za uokoaji. Wanategemewa kwamba watakuja na vifaa maalum pamoja na mbwa wa uokoaji.

Je Obama atapuuza Afrika tena?

8 Novemba, 2012 - Saa 12:08 GMT

Obama na mkewe Michelle
Kuna baadhi ya wenyeji wa bara hili waliotegemea mengi zaidi kutoka kwa mwanawe mtu aliyekuwa akichunga mbuzi huko Magharibi mwa Kenya
Lakini Rais Barack Obama, katika muhula wake wa kwanza, alizuru Afrika mara moja tu, tena kama mpita njia, na kusema wazi kwamba hangekuwa anajihusisha kupita kiasi na maswala ya Afrika.
“Hatima ya Afrika iko mikononi mwa Waafrika wenyewe,” alisema huko Ghana, katika hotuba iliyodhihirisha wazi kwamba ushawishi wa Marekani unapungua katika bara ambalo sasa linafanya biashara zaidi na Uchina kuliko Marekani.
Kwa hivyo, ni mabadiliko yapi yatakayokuwepo katika muhula wa pili?
“Kama Kenya itafanya uchaguzi huru, basi Obama ataitembelea nchi hiyo.''
Swala hili la yeye kutokuwa na muda na Afrika, kwa sababu ya matukio mengine, halikutiwa mkazo katika uchaguzi ulioangazia maswala nyeti nchini Marekani na harakati za mapinduzi katika nchi za Kiarabu.
Akitoa hotuba yake baada ya kushinda, Bwana Obama aligusia tu “,muongo wa vita” na “watu walioko katika nchi za mbali… wanaoweka maisha yao hatarini ili tu kujadili masuala muhimu, na kupata nafasi, kama sisi, kupiga kura kama sisi tulivyopiga leo”
Hakuna “Kanuni za Obama”
Katika muhula wa kwanza, maswala yalilenga mizozo mikubwa iliyokuwa Ivory Coast, Somalia, Sudan and Sudan Kusini, na hata uchaguzi uliofanywa Zambia.
Kuna uwezekano kwamba mwanzo wa muhula wa pili atajishughulisha na masuala kama hayo: mikakati ya kimataifa kuwaondoa waasi wenye uhusiano na Al-Qaeda kutoka Mali kaskazini – kwa kutumia nguvu au mazungumzo, au yote mawili – na juhudi kuhakikisha kuwa Zimbabwe na Kenya hawatakuwa tena na michafuko baada ya uchaguzi, iliyoharibu chaguzi zao zilizopita.
Hadi sasa, hakujawa na ishara yoyote ya kuwepo kwa “Sera Kabambe ya Obama” kwa ajili ya Afrika. Labda hilo siyo jambo baya ukitilia maanani tofauti na masuala mengine kuhusu Afrika.
Rais Barack Obama mjini Washington
Bwana Obama kawaachia wengine watoe tahadhari kuhusu Uchina, nchi ambayo haijitoshelezi kirasilimali.
Lakini kuna uwezekano kwamba muhula wake wa pili utampa nafasi ya kujiondoa kutoka kwa mkakati wake wa “vita dhidi ya ugaidi” huko Mali na Somalia, na kuangazia maswala mapana zaidi – hususan biashara – jambo aliloligusia miaka mitatu iliyopita nchini Ghana.

CAF: orodha fupi ya wachezaji bora soka


 5 Novemba, 2012 - Saa 13:30 GMT
CAF
Wachezaji bora zaidi wa soka barani Afrika watatangazwa na CAF tarehe 20 Desemba
CAF imetangaza orodha fupi ya majina ya wachezaji ambao wamo katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora zaidi barani Afrika.
Mshindi wa mwaka jana, Yaya Toure, anaongoza katika orodha hiyo yenye majina ya wachezaji 10, waliochaguliwa kutoka orodha ndefu ya wachezaji 34.

Mchezaji huyo kutoka Ivory Coast, ambaye ni kiungo cha kati wa timu ya Manchester City, ni kati ya wachezaji wanne wanaozichezea timu za Uingereza ambao huenda wakapata tuzo hiyo ya mwaka 2012.

Kiungo cha kati wa Chelsea, John Obi Mikel, mshambulizi wa Arsenal, Gervinho, Demba Ba wa timu ya Newcastle, ni kati ya wachezaji wengine wa ligi kuu ya Premier ambao wanawania tuzo hiyo.

Katika orodha hiyo, kuna wachezaji wengine ambao waliwahi kucheza Uingereza mwaka 2012.

Wachezaji hao ni aliyekuwa kiungo cha kati wa Arsenal, Alexandre Song, na ambaye sasa huichezea Barcelona ya Uhispania, na mshambulizi wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba, ambaye anaichezea klabu ya China, Shanghai Shenhua.

Chris Katongo ni mchezaji wa pekee kutoka timu ya Zambia iliyoibuka mshindi katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

Mchezaji wa Morocco, Younes Belhanda, yumo katika orodha hiyo, kwa juhudi zake mapema mwaka huu, katika timu ya Ufaransa ya daraja ya kwanza, Montpellier.

Wanaowania tuzo hiyo, watapunguzwa hadi kufikia watatu, katika wiki ya mwisho ya mwezi Novemba.

CAF vilevile ilitangaza orodha fupi ya wachezaji watano, ambao wana nafasi ya kupata tuzo la mchezaji bora barani Afrika, kwa wachezaji ambao hucheza kandanda yao barani Afrika.

Katika ordha hiyo ni pamoja na Mohamed Aboutrika, kiungo cha kati kutoka Misri, na aliyecheza katika mechi ya Al Ahly ya klabu bingwa dhidi ya Esperance ya Tunisia, mchezo uliokwishwa kwa sare ya 1-1 siku ya Jumapili.

Tuzo hizo, ambazo zitakuwa pia ni kumpa zawadi kocha bora zaidi wa mwaka, na klabu bora zaidi mwaka 2012, zitatolewa kwa washindi tarehe 20 mwezi Desemba, katika ukumbi wa Banquet, katika ikulu ya rais, katika mji mkuu wa Ghana, Accra.

Askofu mpya wa kanisa la Kianglikana kutawazwa

Askofu Justin Welby
Askofu wa Durham, Justin Welby, ambaye pia ni mfanyakazi wa zamani katika sekta ya mafuta, anatarajiwa kutajwa kama askofu mpya wa Canterbury.
Inaaminiwa kuwa askofu huyo, mwenye umri wa miaka 56, atateuiliwa kuchukua nafasi ya askofu Rowan Williams, atakayeachia ngazi mwezi Disemba baada ya miaka kumi uongozini.
Askofu Welby, aliteuliwa kama askofu mwaka mmoja uliopita alipochukua wadhifa wa nne kwa ukubwa katika kanisa la kianglikana nchini Uingereza.
Duru kutoka makao makuu ya waziri mkuu nchini humo, zinasema kuwa askofu huyo atatangazwa rasmi siku ya Ijumaa.
Mnamo Jumanne, wadadisi waliwacha kubahatisha kuhusu nani atachukua wadhifa huo baada ya watu wengi kutabiri kuwa yeye ndiye atachukua nafasi ya Rowan Williams
Jarida la Daily Telegraph, lilinukuu kuwa Askofu Welby amekubali kuchukua wadhifa huo ingawa kwa sasa hangeweza kutoa tamko lolote kuhusu udadisi juu yake.
Askofu Welby alisomea chuo kikuu cha Cambridge na kisha kufanya kazi katika sekta ya mafuta kwa miaka kumi na moja kabla ya kusomea dini ambapo baadaye alitawazwa mwaka 1992.

Waasi wadungua ndege ya Khartoum

8 Novemba, 2012 - Saa 17:41 GMT

Mapigano Kordofan Kusini
Waasi katika jimbo la Kordofan Kusini, nchini Sudan wanasema kuwa wamedungua ndege ya kijeshi karibu na mpaka wake na Sudan Kusini.
Msemaji wa kundi la SPLM-North amesema kuwa ndege hiyo ilidunguliwa kufuatia ufyatuaji mkubwa wa risasi katika eneo la milimani la Nuba siku ya Jumatano.
Hakuna tamko lolote kutoka kwa serikali ya Khartoum kuhusu shambulizi hilo.
Waasi wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Sudan katika eneo hilo tangu Juni mwaka jana.
Mzozo huu wa Kordofan Kusini pamoja na Ule wa jimbo la Blue Nile umewafanya maelfu ya watu kutoroka makwao.